Jumatatu , 13th Feb , 2023

Mashaka aliyekuwa mlinzi katika Hoteli ya King iliyopo Kata ya Busresere wilayani Chato ameuawa kwa kupigwa na kitu kichwani usiku wa kuamkia Februari 11, 2023, katika eneo lake la kazi.

Nguo za Mashaka zilizotapakaa damu

Wakizungumzia tukio hilo wafanyakazi wenzake katika hoteli hiyo, wamesema kwamba wao walikuwa wamelala na walivyoamka asubuhi walikuta amelala huku damu zikiwa zimetapakaa kwenye sakafu.

"Nilikuja kuamshwa na mfanyakazi mwenzangu akinipia taarifa kwamba ametoka nje kakuta mlinzi amelala, akijaribu kumsemesha haoneshi ushirikiano, ikabidi tutoke na tulivyotoka tumekuta kweli mlinzi amelala kuangalia vizuri kulikuwa kuna damu zimetapakaa maeneo ya kichwani, hatukuweza kumfunua hatua ya kwanza tuliyochukua ni kwenda Polisi kutoa taarifa, maaskari wakaja kwa ajili ya uchunguzi ikaonekana kwamba mlinzi wetu alikuwa amepigwa na kitu kizito kichwani na kuweza kupoteza maisha," amesema Mnisi.

Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Buseresere amekiri tukio hilo kutokea kwenye Kijiji chake ambapo ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kuwagundua waliofanya tukio hilo kwani hawakuiba chochote baada ya kutekeleza mauaji hayo.

Mganga mfawidhi kituo cha afya Katoro Dokta Zakayo Sungura, amethibitisha kupokea mwili wa marehemu majira ya saa 4:00 asubuhi siku ya Jumamosi ukiwa na majeraha sehemu za kichwani.
Mwenyekiti wa walinzi binafsi mkoa wa Geita Moshi Msimbe akiongea kwa njia ya simu ameiomba serikali kuingilia kati ili mauaji hayo yapungue kwani mpaka sasa wameshafariki walinzi takribani 37 kwenye mkoa wa Geita kwa kipindi cha miaka nane.