Jumamosi , 25th Jun , 2016

Mtu mmoja katika kijiji cha Kitumba tarafa ya Sanjo wilaya ya Magu mkoa wa Mwanza, aliyejulikana kwa jina la Wilson Magola amefariki dunia baada ya kunywa pombe aina ya gongo pamoja na pombe ya ndizi (banana) kupita kiasi bila ya kula chakula.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ahmed Msangi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi Mkoa Mwanza, inadaiwa kuwa marehemu alikuwa akiugua ugonjwa wa kifafa, na siku hiyo mtu huyo alifika nyumbani kwa Bw. Daudi Mtula ambaye anafanya biashara ya kuuza pombe haramu ya gongo, ndipo alipokunywa pombe hiyo iliyopelekea kukosa nguvu hadi kufariki dunia papo hapo.

Aidha, baada ya kufariki dunia, mtuhumiwa Bw. Daudi Mtula aliyemuuzia marehemu pombe hiyo kwa siri alitoroka pamoja na familia yake kusikojulikana na kuacha mwili wa marehemu wenyewe.

Jeshi la polisi lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusiana na tukio hilo na kuweza kufika kwenye eneo la tukio na kuukuta mwili wa marehemu mahali hapo.

Tayari mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi, jeshi la polisi linaendelea na upelelezi pamoja na uchunguzi kuhusiana na kifo hicho, huku msako wa kumtia nguvuni mtuhumiwa aliyemuuzia marehemu pombe hiyo ukiendelea.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ahmed Msangi, anatoa wito kwa wananchi akiwataka kuungana na jeshi la polisi katika kupambana na biashara haramu ya pombe aina ya gongo pamoja na madawa ya kulevya, kwa kutoa taarifa mapema za watu wote wanaojihusisha kwa siri kwenye biashara hiyo.