Ijumaa , 18th Mar , 2016

Watu wanne wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi wameuwawa kwa kupigwa risasi katika majibizano ya risasi na Polisi kwenye msako maalumu unaoendelea kwa ushirikiano wa polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam na mkoa wa Pwani.

Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Kamshna wa Polisi Simon Sirro, amesema kuwa watu wawili wameuawa jijini Dar es Salaam na wengine wawili wameua katika msako kwenye pori la mkuranga baada ya polisi kurushina risasi na watu hao.

Aidha Kamanda Sirro amewataka viongozi wa serikali za mtaa pamoja na wananchi kuwafichua wahalifu hao popote walipo ili kufanikisha kutokomeza uhalifu kwa kuwa jeshi la polisi lenyewe haliwezi kumaliza tatizo hilo bila ushirikiano na jamii inayowazunguka.

Kamanda Siro ameongeza kuwa mbali ya tukio hilo Polisi pia wamebaini kufanyika kwa mafunzo ya kivita kwa watoto kwa kisingizio cha kuwafundisha masuala ya kidini jambo ambalo linakiuka taratibu na sheria za nchi.

Kamanda sirro amesema wanawashikilia watoto takribani 120 kutoka mikoa mbalimbali ambao walipelekwa kwenye pori hilo kwa ajili ya mafunzo ya kidini jambo ambalo linashangaza kwa watoto hao wakiwa chini ya umri wa miaka 18 wameanza kujua kutuamia silaha za kivita.

Katika hatua nyingine Polisi jijini Dar es Salaam wamewakamata watu wanne wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi na silaha mbalimbali za kivita na magari mbalimbali yanayosadikia kutumika katika wizi.