Alhamisi , 3rd Nov , 2016

Msichana wa kazi za ndani Mary Simon (16), mkazi wa Olasiti jana amekutwa amefariki kwa kujinyonga kwa kutumia mtandio aliojifunga kwenye mbao ya kabati la nguo chumbani kwake.

Charles Mkumbo - Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha

 

Akithibitisha leo ofisini kwake, kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Charles Mkumbo amesema tukio hilo lilitokea Novemba 2 mwaka huu, majira ya saa tisa  maeneo ya Olasiti halmashauri ya Jiji la Arusha.

Amesema uchunguzi wa jeshi la Polisi unaonesha kuwa saa saba mchana marehemu alikuwa na watoto wa mwenye nyumba, ambapo walikuwa wakila chakula, ndipo marehemu alipowaeleza wenzake kuwa hakutosheka chakula na kisha kumfuata mtoto mmoja aitwaye Julius Thomas na kumpiga kofi kichwani.

Kamanda Mkumbo ameendelea kusema kuwa mtoto huyo alipomuuliza marehemu sababu za kumpiga kofi, alimjibu samahani na alimrudishia kwa kumpiga kichwani.

Amesema baadaye Mary ambaye ni marehemu aliingia chumbani na kujifungia, baada ya muda kupita simu ya mkononi ya Mary ilikuwa inaita, hivyo Enoth Frank alimpeleka , lakini alikuta mlango umefungwana kuamua kuzunguka dirishani na kuchungulia ndani na akaona Mary ananing’inia kwa kutumia mtandio.

Amesema taarifa zilipowafikia Polisi,walikwenda na kukuta mwili huo na kuupeleka katika hifadhi ya Hospitali ya Mkoa Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi zaidi na chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana, upelelezi unaendelea.