Jumatano , 19th Dec , 2018

Vyama vya Upinzani nchini vimeazimia kuanza kufanya mikutano ya hadhara kwa kile ilichodai kuwa ni kwa mujibu wa haki zao kisheria na kikatiba, hali ambayo inaonekana kuwa tofauti na msimamo wa serikali kuhusu suala hilo.

Edward Lowassa akizungumza kwenye mkutano wa kampeni 2015.

Jana kupitia Mkutano wao na Waandishi wa Habari, uliofanyika Visiwani Zanzibar ambao ulihusisha viongozi mbalimbali wa vyama vya Siasa nchini ikiwemo ACT, Wazalendo, CHADEMA, CUF, Chauma, NCCR-mageuzi pamoja na vyama vingine vya upinzani.

Kupitia mkutano huo, viongozi waliazimia kuanza kufanya mikutano ya siasa na kuwatambua baadhi ya viongozi wao akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko kuwa ni 'wafungwa wa kisiasa'.

"Kama vyama vya siasa vyenye uhalali, na vyenye utaratibu wa rasmi wa kisheria na katiba tutangaza ramsi namna ya kufanya mikutano ya hadhara katika kila kona ya nchi"

Msimamo huo wa vyama vya upinzani unapingana na kauli za mara kwa mara za viongozi mbalimbali wa serikali nchini wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Mawaziri, ambao wamekuwa wakiendeleza msimamo juu ya kuzuia mikutano ya hadhara isipokuwa kwa wabunge wa majimbo husika ambao wameruhusiwa kufanya mikutano hiyo majimboni kwao.

Akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mwezi juni 2016, Rais Magufuli alisema "niwaombe wanasiasa wenzangu tufanye siasa za ushindani baada ya miaka 5 ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi tuliyotekeleza au hatukutekeleza,"

"Ushindani wa sasa unaotakiwa uchukue nguvu ni kwa wale wawakilishi waliopewa nafasi, kama ni wabunge, madiwani na wakajenge hoja kwenye mabaraza yao." aliongeza Rais Magufuli.