Jumatano , 4th Mei , 2016

Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) kimeungana na baadhi ya wadau wake kufanya usafi katika eneo linalotarajiwa kujengwa kituo cha polisi lililopo kijiji cha Msijute jirani na kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Ltd.

Kaimu RPC Mkoa wa Mtwara, George Salala,akiagana na Alhaji Dangote

Akizungumza katika eneo hilo, Mwenyekiti wa MTPC, Hassan Simba, amesema uamuzi wa shughuli hiyo kufanyika katika eneo hilo ni kwa ajili ya kulikumbusha jeshi la Polisi na uongozi wa Dangote ambao ndio ulitoa ahadi ya kujenga kituo hicho kwamba kuna umuhimu wa kuharakisha ujenzi huo ambao kukamilika kwake kutasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa kiwanda pamoja na jamii ya vijiji jirani.

Mwakilishi Mkazi wa Dangote Industries Ltd, Esther Baruti, amewaondoa hofu wakazi wa vijiji hivyo na Mtwara kwa ujumla kwa kuwaambia kuwa tayari ramani kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho imekabidhiwa kwa jeshi la polisi ambao wanasubiri kibali kutoka Makao Makuu ya Jeshi ili ujenzi uanze.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, George Salala, akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa mkoa huo ACP-Henry Mwaibambe, amewaashukuru wanahabari kwa kutambua umuhimu wa kuwapo kwa maendeleo na usalama kwani mambo hayo hayapaswi kwenda tofauti.