Jumapili , 9th Dec , 2018

Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Mahyolo, wilayani Bunda mkoani Mara, Busimba Malegesi, ameonyesha ushujaa wa aina yake baada ya kumwokoa mume wake baada ya kuvamiwa na jambazi mwenye silaha ambaye aliwaingilia usiku nyumbani kwao wakiwa wamelala.

Waziri Lugola alipofika hospitali kumjulia hali, Samson Malegesi aliyekatwa na mapanga baada ya kuvamiwa nyumbani kwake.

Mtu huyo alivamia nyumba hiyo kwa kuvunja mlango, na kuanza kumshambulia mume wa Busimba, Samson Malegesi (62) kwa kumkatakata mapanga mwili mzima.

Busimba alipoona hali hiyo, alimrukia jambazi huyo kiunoni na kumwangusha chini na kumnyang’anya panga pamoja na tochi ambayo alikuwa nayo wakati anamshambulia mumewe.

 “Baada ya kuingia aliwasha tochi na kuanza kumsaka Malegesi, alipomwona alianza kumshambulia kwa kumcharanga mapanga kichwani, mikononi, kwenye mbavu na kusababisha damu nyingi kumwagika", amesimulia mwanamke huyo.

Ameongeza kuwa, "Wakati jambazi huyo akiendelea kumshambulia mume wangu, nilianza kupambana naye ili kumnusuru mume wangu na hatimaye jambazi nilimzidi nguvu kwa kumuangusha chini".

Akiwa katika ziara yake ya kikazi mjini Bunda, Waziri Lugola alimpongeza mwanamke huyo na kumuelezea kuwa ni shujaa kwa kitendo alichokifanya.

Nampongeza sana mwanamke aliyepambana na jambazi na kufanikiwa kumwokoa mume wake. Hakika kama si ushujaa wa mwanamke huyo, mume wake tungempoteza kwa sababu jambazi huyo alidhamiria kumuua kwa kumkata mapanga zile sehemu ambazo ni hatari zaidi kwa uhai wa ubinadamu", amesema Lugola.

"(Mkuu wa Kituo cha Polisi) hakikisheni hamlali mpaka mnalipata hili jambazi kwa kutumia njia zote za kiintelejinsia mlizosomea ili kumkamata haraka iwezekanavyo", ameongeza Lugola.