Jumatatu , 27th Jan , 2020

Kamishina Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Ilala, Janeth Magomi, amethibitisha kifo cha Mwandishi wa Habari, Deogratius David, aliyekutwa amefariki Dunia chumbani kwake, maeneo ya Vingunguti Mji Mpya, huku mwili wake ukiwa umeharibika vibaya.

Mwandishi wa Habari, Deogratius David, wakati wa uhai wake.

Akizungumza na EATV &EA Radio Digital, leo Januari 27, 2020, Kamanda Janeth amesema kuwa, taarifa walizipata kutoka kwa majirani, baada ya kupita siku tatu bila kumuona na kusikia harufu kali ikitoka chumbani mwake na ndipo walipoamua kuvunja mlango.

"Mwili wake ulikutwa umelala kifudifudi kitandani kwake ukiwa umeharibika tayari, majirani wanasema waliamua kuuvunja mlango baada ya kutomuona kwa siku tatu, lakini pia kusikia harufu iliyokuwa ikitokea chumbani mwake na wanasema marehemu alikuwa na ugonjwa wa kifafa" amesema ACP Magomi.

Mwili wa marehemu Deoglatius umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.