
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Mwanza Ahmed Msangi
Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani humo Ahmed Msangi imeeleza kwamba, Mwenyekiti wa huyo wa Mtaa wa Bubale aliyefahamika kwa jina la Alphonce Mussa Nyinzi miaka, 48, aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani na kutokea chini ya kwapa upande wa kulia na watu wawili wasio fahamika.
Risasi hiyo pia ilimjeruhi Neema Marangula miaka 23 Mkazi wa Bulale katika kiganja cha mkono wa kulia.
Imeelezwa kwamba siku ya tukio jana jioni marehemu alikwa ametoka kwenye kikao alichofanya na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mtaa wa Bulale, majira ya saa mbili usiku akielekea nyumbani akiongozana na wajumbe wawili alikutana na Neema Marangula akiwa na mume wake ambao walikuwa wanawafuata marehemu na balozi kwa ajili ya kuzungumzia mzozo wa ndani ya ndoa yao kwa hiyo walikua wanahitaji kusuluhishwa.
Wakati marehemu na wajumbe wake wawili wakiwa pamoja na Bi Neema pamoja na mumewe wakiwa wanajadili tatizo hilo hapo barabarani mara ghafla wakatokea watu wawili ambao walikua wakipita barabarani na kuwaambia mko chini ya ulinzi na mmoja wao akatoa bunduki na kumpiga risasi marehemu ambaye alianguka chini huku wenzake wakikimbia kujiokoa kutoka eneo hilo lakini pia wale wahalifu wakakimbia na kutokomea gizani vichakani.
Kamanda Msangi amesema baada ya tukio hilo ndipo wananchi wa eneo hilo walijitokeza kwa msaada wa kumsaidia marehemu, walimchukua marehemu kumkimbiza hospitali kwa matibabu lakini alifariki dunia wakiwa njiani.
Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Ahmed Msangi anawaomba wananchi wenye taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo zitakazo saidia kufanikisha kukamata wahusika wazitoe polisi. Msako mkali unafanyika kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa.