Jumatano , 22nd Oct , 2014

Mwili wa aliyekuwa Meja Jeneral Herman Corner Lupogo aliyefariki tarehe 19 mwezi huu wa kumi unatarajiwa kuagwa kesho (23/10/2014) katika eneo maalumu la Hospitali Kuu ya Jeshi lugalo jijini Dar es salaam.

Marehemu Lupogo alijiunga na jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania Julai 23 mwaka 1965 na hivyo kuweza kutunukiwa kamisheni Januari 21 mwaka 1966.

Katika utumishi wake enzi za uhai wake alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya mkurugenzi wa mafunzo makao makuu ya jeshi 1971 hadi 1974, katibu msaidizi makao makuu ya chama (ulinzi na usalama) 1974 hadi 1976, mkuu wa chuo cha taifa cha uongozi (Monduli) 1976 hadi 1978.

Marehemu Meja Jeneral Lupogo nimzaliwa wa mkoa wa Ruvuma na amezaliwa Desemba 12 mwaka 1938 wilayani Mbinga mkoani Ruvuma na katika elimu yake aliyoipata aliweza kuhitimu stashahada ya ualimu na shahada ya kwanza ya sanaa katika chuo kikuu cha makerere nchini uganda mwaka 1958 hadi 1964.

Katika utumishi wake alihudhuria kozi mbalimbali ikiwemo ukamanda na unadhimu nchini Canada 1969 na International Strategic studies nchini Uingereza 1985 na amelitumikia jeshi kwa muda wa miaka 28.

Marehemu amefariki akiwa mstaafu ameacha mke na watoto, Mwenyezi mungu ailaze roho ya Meja Jenerali (mstaafu) Hermani Corneli Lupogo mahali Pema Amina.