
Mvutano kati ya Marekani na Venezuela unaongezeka huku meli za kivita za Marekani, USS San Antonio, USS Iwo Jima, na USS Fort Lauderdale zikiwasili Kusini mwa Karibea, hatua ambayo maafisa wa Marekani wanasema inalenga kukabiliana na vitisho kutoka kwa magenge ya madawa ya kulevya ya Amerika Kusini.
Ingawa meli za Walinzi wa Pwani ya Marekani na meli za Jeshi la Wanamaji hufanya kazi mara kwa mara katika Karibea ya Kusini, mkusanyiko huu ni mkubwa zaidi kuliko kawaida kupelekwa katika eneo hilo.
Afisa wa Marekani, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema siku ya jana Alhamisi Agosti 28, kwamba meli saba za kivita za Marekani, pamoja na manowari moja ya mashambulizi ya kasi ya nyuklia, zilikuwa katika eneo hilo au zinatarajiwa kuwepo katika wiki ijayo.
Pentagon haijaonyesha hadharani ni nini hasa ujumbe wa Marekani utakuwa, lakini utawala wa Trump umesema sasa unaweza kutumia majeshi kukabiliana na makundi ya madawa ya kulevya na makundi ya wahalifu na imeiagiza Pentagon kujiandaa kwa lolote.
Nayo Venezuela imelalamikia hatua hiyo jana Alhamisi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ikiishutumu Washington kwa kukiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa ulioanzishwa.
"Diplomasia yetu sio diplomasia ya mizinga, ya vitisho, kwa sababu ulimwengu hauwezi kuwa ulimwengu wa miaka 100 iliyopita," alisema Maduro, ambaye serikali yake ilisema wiki iliyopita itatuma wanajeshi 15,000 katika majimbo ya mpaka wake wa magharibi na Colombia ili kupambana na vikundi vya ulanguzi wa dawa za kulevya.
"Ni operesheni kubwa ya propaganda kuhalalisha kile ambacho wataalam wanakiita hatua ya kinetic ikimaanisha kuingilia kijeshi katika nchi ambayo ni nchi huru na isiyo na tishio kwa mtu yeyote," Balozi wa Venezuela wa Umoja wa Mataifa, Samuel Moncada aliwaambia waandishi wa habari baada ya kukutana na Guterres.
Siku ya Alhamisi, Ikulu ya White House ilisema Trump alikuwa tayari kutumia kila kipengele cha nguvu za Marekani kukomesha dawa za kulevya zisisamike katika nchi nchi ya Marekani. "Mataifa mengi ya Karibea na mataifa mengi katika eneo hilo yamepongeza hatua za utawala za kukabiliana na madawa ya kulevya," katibu wa habari wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt aliwaambia waandishi wa habari.
Jeshi la Marekani pia limekuwa likiendesha ndege za kijasusi za P-8 katika eneo hilo kukusanya taarifa za kijasusi, maafisa wamesema, ingawa zimekuwa zikifanya kazi katika maji ya kimataifa.