Jumatano , 31st Jul , 2019

Kampeni ya Namthamini ya East Africa Television na East Africa Radio, imeendelea kuhakikisha wasichana wote shuleni wanasoma vizuri wakiwa wanapata taulo za kike.

Leo Julai 31, 2019 timu ya Namthamini imefika wilayani Hanang katika shule ya Sekondari Simbay, iliyopo takribani Kilometa 30 kutoka mjini na kukabidhi Pedi kwaajili ya wasichana 114 ambazo watazitumia kwa mwaka mzima.

Akiongea wakati wa kupokea taulo hizo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang Joseph Mkirikiti amesema Kampeni ya Namthamini ya East Africa Television imesaidia kuongeza ufaulu kwasababu inawasaidia wanafunzi kusoma bila kukosa masomo.

"Niwashukuru East Africa Television kupitia kampeni hii naamini ufaulu utaongezeka kwa wasichana maana mmetatua changamoto yao kubwa inayowafanya wakose masomo", amesema Mkirikiti.

Kwa upande wake Mwalimu wa taaluma Madam Christina, akiongea kwa niaba ya mkuu wa shule hiyo ameeleza kupokea kwa furaha msaada huo na kusema kuwa suala la hedhi huwa linachangia utoro kwa wanafunzi.

"Sasa naamini wanafunzi wangu watafaulu kwasababu nitawaona shuleni siku zote tutaondokana na ruhusa kwasababu ya hedhi ambazo zilikuwa zinawafanya mkose mtiririko wa vipindi", amesema.

Shule ya Simbay ni shule ya kutwa yenye jumla ya wanafunzi 207, Wavulana wakiwa ni 94 na wasichana 114.