Alhamisi , 10th Dec , 2015

Halmashauri ya mji wa Nanyamba mkoani Mtwara inakabiliwa na deni la zaidi ya sh. Milioni 242.5 kutokana na kupokea watumishi na wakuu wa idara wapya toka ilipopata hadhi ya halmashauri mwezi Julai mwaka huu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nanyamba, Oscar Ng’itu.

Akizungumza katika uchaguzi wa kuwachagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa halmashauri, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Oscar Ng’itu, amesema miongoni mwa mambo yanayopelekea madeni ni ununuzi wa Samani na ukarabati wa majengo ambapo kwa sasa wanatumia ofisi za kata.

Aidha, amesema, halmashauri inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwa ni pamoja na rasilimali watu na uhaba wa magari, kutokana na kuwa na magari sita ambayo hata hivyo yanahitaji fedha kwa ajili ya ukarabati.

Ng'itu ameongeza kuwa magari waliyopewa kwa ajili ya shughuli za kiofisi hayapo katika hali nzuri kiasi cha kuweza kuhimili mikikimikiki ya shughuli za kimaendeleo katika Halmshauri hiyo.