Jumanne , 10th Sep , 2019

Mbunge wa Mtama Mkoani Lindi Nape Nnauye, amemuomba msamaha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, hii ikiwa ni miezi kadhaa imepita tangu kusikika kwa sauti yake na viongozi wengine wa siasa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zenye maneno yasiyofaa.

Rais Magufuli (kulia) na Nape Nnauye (kushoto).

Mbunge Nape amekutana na Rais Magufuli leo Septemba 10, 2019, Ikulu ya Dar es Salam, ambapo mara baada ya mazungumzo yao amemshukuru Rais kwa kukubali kukutana naye na kumsamehe.

''Kwanza nimekuja kumuona kama Baba yangu, kwa sababu wote mnajua yametokea mambo mengi hapa katikati na mimi kama mtoto wa CCM, mimi kama mwanaye nilidhani ni vizuri nije niongee na Baba yangu na namshukuru kwamba alinipa fursa ya kumuona na ameniambia amenisamehe'' amesema Nape.

Kwa upande wake Rais Magufuli amesema, Nape amekuwa akiomba kukutana nae mara nyingi kupitia kwa watu mbalimbali wakiwemo wasaidizi wake, viongozi wastaafu na viongozi wa CCM na kwamba baada ya kukutana nae na kumuomba radhi ameamua kumsahehe.

''Kikubwa anachozungumza naomba Baba unisamehe,  kwahiyo inauma kusamehe kunaumiza lakini nasema kwa dhati nimemsamehe'', amesema Rais Magufuli.

Ikumbukwe kuwa Rais Magufuli amemsamehe Nape ikiwa ni siku chache tu, tangu alipotangaza kuwasamehe wabunge William Ngeleja na January Makamba.
 

Zaidi Tazama video hapo chini