Alhamisi , 21st Mei , 2020

Chama cha NCCR Mageuzi kimewapokea wanachama takribani 90,000 kutoka vyama mbalimbali vya siasa katika mikoa ya Shinyanga na Mara, akiwemo aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga, ambao wamevihama vyama vyao.

Wanachama wapywa wa NCCR Mageuzi mkoani Shinyanga

Akizungumza na wanahabari Mjini Shinyanga baada ya kupokea wanachama wapya zaidi ya 12,000 kutoka Jimbo la Shinyanga, Mkuu wa Idara ya Uenezi wa NCCR Mageuzi nchini, Edward Simbeye amesema kuwa mkoa wa Mara una wanachama 48,000 na mkoa wa Shinyanga ukiwa na wanachama 42,000.

"Ukijumlisha kwa mikoa hii miwili tu, tuna wanachama 90,000, mkoa wa Mara tuna wanachama 48,000 na mkoa wa Shinyanga kwa mujibu wa mwakilishi wetu aliyekuwa akiendesha zoezi hili, tuna wanachama 42,000", amesema Simbeye.

Naye aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga, Shigano Charles Mapema akitangaza kukihama chama hicho pamoja na mwenzake aliyewahi kuhudumu kitengo cha Operesheni ya Chadema ni Msingi, Majimbo ya Solwa, Kongwa na Temeke, Yunis Kanumba wamesema kuwa hawajaridhishwa na jinsi CHADEMA inavyowafanyia baadhi ya wabunge wake.

Baadaye Mkuu wa Idara ya Uenezi wa NCCR Mageuzi nchini, Edward Simbeye akaweka wazi msimamo wa chama chake kuwa kimejipanga kusimamisha mgombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.