"Nimesafisha Dar, sasa naingia chumbani " -Waitara

Jumatatu , 29th Jun , 2020

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara, amesema kuwa mpaka sasa hivi amekwishamaliza kazi kubwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam ya kukisambaratisha Chama cha CHADEMA, na kwa sasa ataingia chumbani kwenye Jimbo la Tarime Vijijini lililokuwa likiongozwa na John Heche

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara

Waitara ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kusema kuwa tangu alipoamua kubadili upepo wa  chama cha siasa, alipanga pia kubadilisha jimbo na hivyo msimamo wake uko palepale na Julai 14,  ataenda kuchukua fomu ya Ubunge kupitia CCM kwenye jimbo la Tarime Vijijini

"Dar es Salaam sina ninayemkimbia jimbo langu la Ukonga liko salama kuanzia ndani na nje ya chama, nimeshafanya kazi ya kuwasambaratisha CHADEMA hawapo kabisa  walikuwa na Meya wa Jiji hayupo, Meya wa Ilala hayupo, mimi nimeshamaliza kazi Dar es Salaam naamini nimefyeka kwenye Sebule, nadhani chumbani ndiyo kuna tatizo hivyo nitafanya siasa mkoani Mara kwenye Jimbo la Tarime Vijijini" amesema Naibu Waziri Waitara.