Alhamisi , 15th Dec , 2016

Katibu Mpya wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole amesema atahakikisha chama hicho hicho kinakuwa ni cha wanyonge na kuendelea kuwa kimbilio la wasio na sauti.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole akizungumza wakati wa makabidhiano rasmi na Katibu Mwenezi Mstaafu wa CCM, Nape Nnauye (kulia), leo katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Polepole ametoa kauli hiyo leo wakati akikabidhiwa rasmi ofisi na mtangulizi wake Nape Nnauye katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam, na kusema kuwa msingi wa chama hicho ni utetezi wa wanyonge.

Pia Polepole amesema katika kutekeleza majukumu hayo mapya aliyokabidhiwa atahakikisha atajikita zaidi katika kazi ya itikadi zaidi kuliko uenezi kwa kuwa itikadi ndiyo inayokibeba chama.

"Msingi wa chama chetu ni utetezi wa wanyonge, tutahakikisha kinaendelea kuwa kimbilio la wasio na sauti. Nafasi hii ina mambo mawili ITIKADI na UENEZI, tutafanya uenezi lakini tutajikita zaidi kwenye itikadi ili kusimamia misingi" amesema Polepole.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wakuu wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa halmashauri kuu kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo.

Polepole amemsifu Nape kwamba aliongoza Idara hiyo vizuri na kwa hiyo anaendelea kuhitaji ushauri wake katika kazi zake.
Pia Polepole ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo amesema, atafanya kazi kwa weledi mkubwa  huku akiahidi kushirikiana kwa karibu na waandishi wa habari.