Jumatatu , 10th Aug , 2020

Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kati Lazaro Nyalandu leo Agosti 10, 2020, amejitosa kwenye kinyang'anyiro cha kumpata mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia chama hicho, ambapo mchakato wa kura za maoni unaendelea sasa hivi.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, Nyalandu amewashukuru wale wote wanaomuonesha upendo na kwamba matokeo ya uchaguzi huo yatashuhudiwa na Mgombea Urais wa chama hicho Tundu Lissu. 

"Nitashiriki kama mgombea katika kinyang'anyiro cha kumpata mgombea Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA Jimbo la Singida Kaskazini, Uchaguzi huo utafanyika leo, Jumatatu, Agosti 10, kijijini Ilongero, Asanteni sana kwa sala na dua zenu, na zaidi kwa upendo wenu wa daima kwangu", ameandika Nyalandu.

Aidha Nyalandu ameongeza kuwa, "Nimempokea Mh Tundu Lissu, jimboni Singida Kaskazini sasa hivi, Mh Lissu atashuhudia matokeo ya Ubunge Singida Kaskazini, mchuano baina yangu na David Jumbe kumpata Mgombea  wa Chama chetu 2020".

Awali Nyalandu aliomba ridhaa ya chama chake kimteue kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao, ambapo chama hicho kilimpa ridhaa Tundu Lissu.