Jumanne , 19th Mei , 2015

Rais wa Msumbiji Fellipe Jacinto Nyusi leo amelihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amesema ziara yake imelenga kuja kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya mataifa haya mawili tangu enzi za harakati za ukombozi.

Rais wa Msumbiji Filepe Jacinto Nyusi

Rais Nyusi amesema hayo leo wakati alikilihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini ambapo amesema siku zote maendeleo ya nchi yanatokana na uhusiano mzuri baina ya nchi na nchi.

Bw. Nyusi ambaye anakuwa Rais wa kwanza wa Msumbiji kuhutubia bunge la Tanzania, amesema kuwa mbali na ushirikiano mzuri wa kisiasa angependa kuendeleza ushirikiano wa kibiashara, elimu na katika nyanja nyingine mbalimbali.

Rais Nyusi ambaye aliingia nchini Juzi ameshafanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, kisha akaelekea visiwani Zanzibar ambapo alikutana na Rais wa visiwa hivyo Dkt, Ali Mohammed Shein na leo amemalizia ziara yake Bungeni mjini Dodoma.

Katika hotuba, Rais Nyusi pia ameahidi kushirikiana na Tanzania katika ulinzi wa amani pamoja na vita dhidi ya ugaidi katika mataifa ya Afrika.

Kwa upande wake spika wa bunge la Muungano Mh. Anne Makinda amesema kuwa ni heshima kubwa kwa Rais huyo wa kwanza wa msumbiji kuhutubia bunge na kuongeza wataendelea kukuza uhusiano baina ya nchi hizo ili kuleta maendeleo ya nchi hizo.

Makinda amesema kumekuwa na uhusiano mzuri wa kisiasa ambao kwa sasa wataendeleza mshikamano kati ya wabunge wa Tanzania na Msumbuji ili kuboresha maisha ya wananchi wa nchiu zote mbili.