Ole Sabaya aeleza alivyoamuru Mbowe alindwe

Jumanne , 8th Oct , 2019

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema kitendo alichokifanya cha kuwatuma askari Polisi kuingia kwenye Mkutano wa CHADEMA, kilikuwa sawa na alifanya hivyo lengo lake ni kumlinda Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe.

Lengai Ole Sabaya ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam, wakati akizungumzia uamuzi wa kuagiza Askari wa Jeshi la Polisi kuingia kwenye kikao cha ndani cha CHADEMA, na kusema uamuzi wake ulikuwa sahihi.

"Niliwatuma Askari waingie mkutano wa ndani wa CHADEMA, na niliwaambia wakae ndani ya hicho kikao ila sikuwaambia wavunje mkutano, wao ni chombo cha dola, hata wakija hapa kwenye ofisi zenu sio tatizo."

"Namimi nadhani walipaswa kunipongeza, kwa sababu niliamuru Mwenyekiti wao Freeman Mbowe  alindwe, ila kwa sababu wao ndiyo wamekuwa na mashaka kila wakati ndiyo maana wanalalamika kila mara", ameongeza Ole Sabaya.

Hivi karibuni wilayani Hai, DC Ole Sabaya aliamuru askari polisi mkoani Hai kuingia ndani ya kikao cha ndani cha CHADEMA huku CHADEMA wenyewe wakilalamika kitendo hicho si sawa.