Jumapili , 31st Aug , 2025

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili katika mji wa bandari wa kaskazini mwa China wa Tianjin leo Jumapili katika mkutano wa kilele wa usalama wa kikanda ambao China inatarajia kuutumia kukabiliana na ushawishi wa Magharibi katika masuala ya kimataifa.

Katika ziara hiyo isiyo ya kawaida ya siku nne kwa jirani na mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Urusi, Putin anaendeleza uhusiano kati ya China na Urusi unaotajwa kuwa bora zaidi katika historia, baada ya kuwa imara zaidi, kukomaa na muhimu kimkakati kati ya nchi kubwa, shirika la utangazaji la serikali ya China CCTV limeripoti.

Rais Xi Jinping atakuwa mwenyeji wa takriban viongozi 20 wa dunia mjini Tianjin, akiwemo pia Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, katika mkutano wa kilele wa siku mbili wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai, mkutano mkubwa zaidi tangu kundi hilo lianzishwe mwaka 2001 kati ya mataifa sita ya Eurasia.

Umoja huo unaozingatia usalama umepanuka na kufikia wanachama 10 wa kudumu na nchi 16 zikiwa kwenye mazungumzo ya kujiunga na waangalizi katika miaka ya hivi karibuni. Utume wake umeongezeka kutoka katika usalama na kukabiliana na ugaidi hadi ushirikiano wa kiuchumi na kijeshi.

Siku moja kabla ya ziara yake, Putin alikashifu vikwazo vya nchi za Magharibi katika mahojiano yaliyoandikwa na shirika rasmi la habari la China Xinhua, akisema Moscow na Beijing kwa pamoja zinapinga vikwazo vya kibaguzi katika biashara ya kimataifa. Uchumi wa Urusi uko ukingoni mwa mdororo, kwa sababu ya vikwazo vya biashara na gharama ya vita vyake nchini Ukraine.

Viongozi kutoka Asia ya Kati, Mashariki ya Kati, Asia ya Kusini na Kusini-mashariki mwa Asia watahudhuria mkutano huo katika kile China inalenga kuonyesha kuwa ni maonyesho yenye nguvu ya umoja kati ya Global South, wakirejelea nchi zinazoendelea na zenye kipato cha chini, nyingi zikiwa katika ukanda wa kusini mwa dunia.