Jumanne , 13th Jul , 2021

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameusisitiza uongozi wa Mkoa wa Pwani kutumia mkakati wa uvunaji wa mifugo kama mkakati wa kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima pamoja na kuondokana na tatizo la uhaba wa malighafi katika viwanda vya kuchakata nyama mkoani humo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega

Mhe. Ulega amesema hayo alipokutana na uongozi wa mkoa huo ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Abubakar Kunenge, akitoa taarifa ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani, na kufafanua kuwa ni ni vyema uongozi huo ukafanya tathmini ya kina kwa kuunda kamati maalum ili kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji mkoani humo.

Amesema serikali inalichukulia suala hilo kwa uzito mkubwa hivyo ni vyema viongozi ndani ya mikoa yote nchini wakaunda kamati maalum za wataalamu kwenda wilayani hadi vijijini ili kutafuta ufumbuzi wa haraka na kudumu.
 
Akizungumzia hali halisi ya hatua zilizochukuliwa na Mkoa huo kukabiliana na kero hiyo RC Kunenge amewataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kutochukua sheria mkononi na kuviasa vyombo vya ulinzi na usalama kutenda haki wanapopata taarifa ya migogoro hiyo, huku akifafanua kuwa tayari wameanza kufanya sensa ya mifugo katika wilaya zote na Wilaya ya Rufiji kwa sasa ipo hatua za mwisho kukabidhi mapendekezo yao.

Katika hatua nyingine Mhe. Ulega ameagiza uongozi Taasisi ya Chanjo Tanzania TVI pamoja na wizara wanaohusika na masuala ya chanjo kuhakikisha chanjo zinazozalishwa na taasisi hiyo zinawafikia wafugaji waliopo vijijini badala ya kuanza kufikiria kusambaza chanjo hizo nje ya nchi.
 
Mhe. Ulega amesema kuna mifugo mingi kama kuku, ng'ombe na mbuzi wanaokufa kwa kuwa wafugaji hawajui kama kuna chanjo zinazozalishwa hapa nchini ingawa kuna maeneo mengine chanjo hizo hazijafika kabisa hivyo amewataka viongozi hao kuhakikisha chanjo zinafika maeneo mbalimbali nchini hususan vijijini ili wafugaji waweze kukinga mifugo yao dhidi ya magonjwa mbalimbali.