Jumatano , 3rd Jun , 2015

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mbunge wa Ukonga, Eugenia Mwaiposya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshutuko na masikitiko taarifa za kifo cha mbunge wa Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, Mheshimiwa Eugenia Mwaiposya ambaye ameaga dunia usiku wa kuamkia leo, Jumanne, Juni 2, 2015, mjini Dodoma ambako alikuwa anahudhuria Vikao vya Bunge.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Makinda, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshutuko na masikitiko taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Eugenia Mwaiposya ambaye nimejulishwa ameaga dunia mjini Dodoma ambako alikuwa anaendelea kuhudhuria Vikao vya Bunge.”

Amesema Rais Kikwete: “Kwa hakika, taifa letu limepoteza kiongozi muhimu kutokana na kifo hiki. Mbunge Mwaiposya alikuwa mwakilishi hodari na mtetezi wa kuaminika wa wananchi wa Jimbo la Ukonga. Napenda kukutumia wewe Mheshimiwa Spika salamu zangu za rambirambi kwa kupoteza Mbunge mahiri sana. Aidha, kupitia kwako, nawatumia Wabunge wote salamu zangu za rambirambi kwa kuondokewa na mwenzao.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Kupitia kwako, Mheshimiwa Spika, napenda pia kutuma salamu zangu kwa wananchi wa Jimbo la Ukonga ambao wamepoteza mwakilishi wao. Mheshimiwa vile vile, napenda kutoa pole nyingi kwa familia, ndugu na jamaa wa Mbunge Mwaiposya kwa kuondokewa na mama na mchangiaji mkubwa katika maisha yao. Wajulishe niko nao katika msiba huu mkubwa. Naelewa uchungu wao katika kipindi hiki na nawaombea subira ili waweze kuvuka kipindi hiki. Naomboleza nao na naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Mheshimiwa Eugenia Mwaiposya. Amina.”