Jumatatu , 15th Jul , 2019

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Julai 15, amezindua nyumba takribani 20 za Askari Polisi, eneo la Magogo Mkoani Geita, na kumtaka Kamanda wa Polisi nchini, IGP Simon Sirro kuwa mkali zaidi.

Rais Magufuli na IGP, Simon Sirro

Rais Magufuli amesema kuwa kuna mambo mengi si ya kiuadilifu bado yanaendelea katika jeshi hilo ambayo yanahitaji kushughulikiwa huku pia akimpomgeza IGP kwa hatua za kinidhamu anazochukua kwa askari ambao sio waadilifu, ambapo kwa kipindi cha mwezi Januari hadi June
2019, jumla ya Askari 54 wamefukuzwa kazi.

''Endelea kuwa mkali ili kuimarisha nidhamu katika jeshi, ukweli ukitaka kazi ziende vizuri kufukuza kupo, wapo watu wanaobambikiza kesi, wapo maaskari wanaohusika katika ujambazi lakini hawa ni wachache sana'', amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli akimjibu IGP Sirro, juu ya nyumba hizo za maaskari kupewa jina lake, Rais Magufuli akamgeuzia kibao IGP, ambapo amesema, "IGP umeomba hii Barracks iitwe jina langu, ila mimi nataka iitwe Sirro Barrack, ili uisimamie vizuri na ujenzi ukishindwa kukamilika aibu ibaki kwako''.

Pia Rais Magufuli ameendelea kusisitiza amani, na kuwataka viongozi mbalimbali kuendelea kuitunza na kuilinda amani ya nchi iliyopo.