Jaji wa Mahakama Kuu Alexandre de Moraes, aliyeongoza kesi hiyo aliatoa uamuzi wa kumbakisha Bolsonaro kizuizini baada ya kukamatwa mapema Jumamosi.
Bolsonaro hatakaribiana na wafungwa wengine wachache wanaozuiwa katika makao makuu ya polisi ya shirikisho.
Jaji De Moraes alichukua uamuzi huo wakati upande wa utetezi ukiwa umemaliza rufaa zote. Hata hivyo, mawakili wa Bolsonaro wameahidi kuendelea kuwasilisha maombi ya kifungo cha nyumbani kutokana na afya mbaya ya kiongozi huyo wa zamani.
Bolsonaro na washirika wake kadhaa walihukumiwa na mahakama hiyo kwa kujaribu kuipindua demokrasia ya Brazil baada ya kushindwa na Rais Luiz Inácio Lula da Silva kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Mapinduzi aliyoyapanga yalijumuisha mipango ya kutaka kumuua Lula na kuchochea uasi mwanzoni mwa mwaka 2023. Alikutwa pia na hatia ya kuongoza genge la uhalifu na kujaribu kuuondoa utawala wa sheria unaofuata demokrasia.
Jumamosi ya wiki iliyopita Mstaafu Jair Bolsonaro alikamatwa na polisi siku kadhaa kabla ya kuanza kutumikia kifungo cha miaka 27 jela
Jaji Alexandre de Moraes wa Mahakama Kuu ya Brazil amesema Bolsonaro alikamatwa kwasababu ya hatari iliyosababishwa na wafuasi wake kwa kuwazuia polisi waliokuwa wakimfuatilia.
Alibainisha pia kuwa kulikuwa na ushahidi wa kujaribu kukihujumu kifaa cha kufuatilia mwenendo wa Bolsonaro alichokuwa amefungwa mguuni.




