RC aeleza kufungwa kwa mipaka kulivyoleta chuki

Jumanne , 19th Mei , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigella, amesema kuwa kitendo cha Watanzania kuzuiliwa kuingia nchini Kenya, kimeleta chuki kubwa kati ya wananchi wanaoishi katika mpaka wa Horohoro na kuona kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa na busara za wao kuendelea kuwaruhusu Wakenya kuja nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella.

RC Shigella ameyabainisha hayo leo Mei 19, 2020, kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio na kusema kuwa hiyo nayo ni moja ya sababu ya kuzuia Wakenya, wanaopitia mpaka wa Horohoro kuingia nchini kwa sababu hata wao, wana maambukizi ya Virusi vya Corona, kama ambavyo wamekuwa wakiwatangaza Watanzania kuwa wana maambukizi.

"Walio wengi wanapata huduma huku kwetu kuliko Watanzania wanaopata huduma Mombasa na hii imeleta chuki kati ya wananchi walioupande wa Horohoro na Mombasa, wanaona kwamba sisi tumekuwa na busara sana, haiwezekani walioko upande wa Horohoro wazuiliwe kwenda Kenya halafu wao waruhusiwe kuja kwetu ili hali na wao wana Corona hivyo na sisi wanatuletea maambukizi" amesema RC Tanga.

Aidha akizungumzia wale madereva ambao ni raia wa Kenya, lakini wanasafirisha mizigo kupeleka maeneo mengine kama Congo, RC Shigella amesema, "Hatutaruhusu Mkenya anayepita ndani ya nchi yetu kuelekea nchi zingine za Zambia ama Congo, kwa sababu tunaushahidi wa kutosha kwamba walio wengi wana maambukizi ya Virusi vya Corona".