Jumatano , 7th Apr , 2021

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira amesema tangu kuchaguliwa kuwa mkuu wa mkoa huo ameshakutana na hali ya kudharauliwa kutokana na yeye kuwa mwanamke ndani ya uongozi.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira

Akizungumza katika kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio RC Mghirwa amebainisha kilichotokea katika kikao chake cha kwanza akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanajaro na adhaa aliyokutana nayo.

"Kikao changu cha kwanza  tangu siku tatu nimeingia nikiwa RC Kilimanajario, mjumbe mmoja kiongozi mwanaume akasimama akaniambia, mimi siwezi kukupa wewe mawazo yangu kwa sababu wewe si wachama changu, Nikamwambia huu si mkutano wa chama wala mimi sio Mwenyekiti wa chama na hapa ni serikalini, hii imetokea mara nyingi mwingine siku moja aliniambia utanitambua leo lakini mimi ukinidharau huwa hainusumbui," alisema RC Mghwira.

Akielezea kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu, iliyosema kuwa macho yake yanaona, amesema kwenye uumbaji Mungu alimpa mwanamke fikra au macho ya ndani ambayo yana umuhimu kwenye uongozi.

"Hayo macho aliyokuwa anayasema sio haya magoroli tulionayao ni yale macho ya ndani, macho ya utambuzi, macho ya nafasi, hayo macho ya nafasi wanayo wanawake zaidi wanaume kidogo, wanawake tuyatumie vizuri yatasaidia jamii," alisema RC Mghwira.