Jumanne , 30th Aug , 2022

Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa, amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, kukutana na wadau na wamiliki wa mabasi ili kuweka utaratibu mzuri ambao ni shirikishi wa utoaji huduma kwa wananchi kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli jijini humo.

Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa

Bashugwa ametoa maelekezo hayo leo Agosti, 30, 2022 wakati akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya utoaji wa huduma kwa wananchi wanaoingia mkoa wa Dar es Salaam kupitia kituo kikuu cha mabasi cha magufuli.

"Kuna abiria wanaoingia mkoa Dar es Salaam na kushushwa katika stendi ya Magufuli lakini wanahitaji mabasi hayo yawafikishe mjini kwenye vituo vya mabasi vilivyojengwa na sekta binafsi, kwahiyo mkuu wa mkoa akikutana na wadau hao wataona namna nzuri ya kusimamia suala hilo" amesema Bashungwa

Aidha, Bashungwa amemtaka RC Makalla kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na wadau wengine ili kukubaliana na kuweka utaratibu utakaorahisisha utoaji wa huduma bora bila kuleta adha kwa wananchi wala kuathiri malengo ya serikali kujenga stendi hiyo.