Alhamisi , 24th Mar , 2016

Sakata la baadhi ya Wenyeviti wa Kamati za kudumu na Makamu wenyeviti kudaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa limechukua sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU), kuanza rasmi kulichunguza.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Valentino Mlowola

Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari jana ofisi hiyo ya kupambana na rushwa imesema kuwa taarifa hizo za rushwa zimeshaifikia ofisi hiyo na tayari wameshaanza kuzishughulikia.

Hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa tuhuma za rushwa kwa baadhi ya viongozi wa kamati za bunge huku wabunge wengine wakijiuzulu kwa kutaka mamlaka za kiuchunguzi zichunguze tuhuma hizo ili sheria ichukue mkondo wake

Taarifa hiyo iliyotolewa na Takukuru imesema kuwa taasisi hiyo ndio yenye dhamana ya kuchunguza tuhuma zote zinazohusu rushwa kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia na kupambana na rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Wakati huo huo, Chama cha Act-Wazalendo kimemtaka Spika wa Bunge la Muungano Job Ndugai kufanya uchunguzi kwa kamati zote zilizotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kubaini ukweli na hatua kisheria zichukuliwe.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jana Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya bunge na serikali za Mitaa wa ACT-Wazalendo, Yeremia Maganja amesema kama Spika hataonyesha kuchukizwa na rushwa atakuwa hajawatendea haki watanzania

Mwenyekiti huyo amesema kuwa kashfa hizo zimeliondolea heshima bunge wakiwemo wabunge kwa sababu ni chombo chenye madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake juu ya utekelezaji wa majukumu yake.