Ijumaa , 7th Nov , 2014

Wabunge David Kafulila na Zitto Kabwe waitaka serikali kuzuia malipo ambayo kampuni ya IPTL inaendelea kulipwa zaidi ya Bilion 12 kila mwezi, hadi Taarifa ya uchunguzi wa tuhuma za UFISADI katika akaunti ya ESCROW itakapowekwa hadharani,

Sakata ya ufisadi wa bilioni 200 fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow limeingia katika sura mpya baada ya baadhi ya wabunge kuomba mwongozo unaolitaka shirika la umeme nchni –TANESCO – kusitisha kulipa shilingi Bilioni 12 kila mwezi kwa watuhumiwa wanaochunguzwa kwa wizi mpaka uchunguzi utakapokamilika.

Wakiomba mwongozo wa spika katika mkutano wa kumi na sita kikao cha Nne cha Bunge, mbunge wa kigoma kusini Mhe. David Kafulila amehoji sababu za serikali ya kutochukua hatua ya kuzuia fedha hizo kama ambavyo benki ya Uholanzi ilivyoamua kuzuia fedha hizo kwa kuitikia wito wa Bunge la Tanzania mpaka uchunguzi utakapokamilika.

Akitolea ufafanuzi Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Mhe. William Lukuvi amesema taarifa hizo kutoka nje ya nchi serikali haijazipata na kusisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania sakata la IPTL na Escrow akaunti linashughulikiwa na taasisi mbili ikiwemo ya TAKUKURU na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Aidha bunge limeingia katika siku ya Nne ya kujadili na kuishauri serikali juu ya mapendekezo ya utekelezaji wa mpango wa taifa kwa mwaka 2015/2016.