Alhamisi , 8th Jun , 2017

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu ametoa agizo kwa mawaziri wawili wa Ardhi , William Lukuvi na Waziri wa Afya,  Ummy Mwalimu kufika mkoani Mara haraka iwezekanavyo kutatua changamoto za sekta ya afya na migogoro ya ardhi ambayo ni kero kubwa.

Makamu wa Rais Samia Suluhu

Samia ametoa agizo hilo akiwa kijijini Butiama na viongozi wa mkoa wa Mara katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.

Mh. Suluhu amesema kwamba katika ziara yake mkoani Mara wananchi wamelalamikia mno kuwepo kwa  migogoro ya ardhi kati  ya kijiji na kijiji na kusuasua kwa utoaji wa  huduma za afya kutokana na baadhi ya hospitali kukosa fedha kutoka Serikalini jambo ambalo litapatiwa ufumbuzi na Waziri husika pindi watakapofika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt Charles Mlingwa amemshukuru Makamu wa Rais kwa ziara hiyo ya kikazi mkoani humo na amemuahidi kuwa maelekezo na maagizo aliyoyatoa yeye pamoja na watendaji wa wilaya zote za mkoa wa Mara watayatekeleza kwa uhakika.