Jumatatu , 20th Mei , 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema kuwa hakuna bodaboda yoyote itakayokamatwa isipokuwa zilizohusika katika ajali, uhalifu na pikipiki ambazo hazina mwenyewe.

Waziri Kangi Lugola.

Waziri Kangi ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo Mei 20, wakati akijibu swali la Mbunge viti maalum (CCM) kutoka mkoani Tabora Rehema Migila, ambaye alihoji kuwa kumekuwa na ukamataji wa bodaboda kiholela na zinaporudishwa kwa wamiliki huwa zimechomolewa baadhi ya vifaa na zingine hubambikiziwa kesi kubwa na wamiliki kuzitelekeza.

Kangi amesema kuwa hakuna bodaboda itakayokamatwa kwa makosa ya mwendokasi au kutovaa kofia ngumu (helmet) isipokuwa pikipiki iliyotumika katika uhalifu, iliyopata ajali na bodaboda ambayo haina mwenyewe.

"Hakuna bodaboda itakayokamatwa kama haiko katika makundi hayo matatu, hakuna atakayepelekwa kituo cha polisi kwa makosa madogo madogo, sasa hivi bodaboda nchi nzima wanakula raha tu", amesema Waziri Kangi.

Hayo yamejiri baada ya bodaboda nyingi kukamatwa na kupelekwa katika vituo vya polisi, hali ambayo hupelekea madereva wengi kuzitelekeza vituoni kutokana na kushindwa kuzilipia faini.