Alhamisi , 31st Mar , 2016

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki amesema serikali imeanza kufanyia kazi marekebisho ya utaratibu wa utoaji hati za kimila ambazo zimeonekana bado ni changamoto na chanzo cha migogoro.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki.

Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na Tamisemi pamoja na uongozi wa Mpango wa Kurasimisha Biashara za Wanyonge (MKURABITA) na kuongeza ofisi yake itahakikisha mpango huo unainua vipato na kuwainua wanyonge sambamba na kuwanufaisha watanzania wote bila ubaguzi.

Mhe Kairuki amesema ofisi yake inashirikiana na taasisi zingine zinazohusika na vibali mbalimbali kutambua uhalali kwa baadhi ya watu ambao wamekua wakijitokeza kwa madai mbalimbali hasa yale madai ya ardhi ambayo yanahusisha masuala ya uzalishaji mali kama ya Kilimo na kupunguza hali ya migogoro isiendelee kutokea..

Aidha Waziri Kairuki ameongeza kuwa licha ya urasimishaji wa ardhi ba biashara imetakiwa kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi hususani wafanyabiashara ili waweze kulipa kodi stahili kutokana na faida wanayoipata.

Waziri huyo wa Utawala bora amesema kuwa April Mosi mwaka huu, Mkurabita wataanza shughuli ya urasimashaji ardhi katika mikoa ya Iringa na Morogoro ili hatia zitakazotolewa wananchi waweze kuzitumia kama dhamana.