Jumatano , 4th Feb , 2015

Bunge kupitia kamati yake ya Uongozi limeiagiza serikali kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya utoaji elimu na uandikishaji wapiga Kura katika daftari la Kudumu la wapiga Kura kwa mfumo wa BVR.

Mwenyekiti wa Bunge Mussa Azzan

Akitoa taarifa ya mwenyekiti leo Bungeni wakati wa kuahirisha kikao cha 8 cha mkutano 18 wa bunge, mwenyekiti wa Bunge Mussa Azzan amesema kuwa Serikali imeridhia kutoa fedha kwa kadri ya mahitaji ya tume ya taifa ya uchaguzi inayosimamia zoezi hilo.

Maamuzi hayo yametokana na hoja ya mbunge James Mbatia aliyetaka bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili suala hilo kama jambo muhimu na la dharura.

Azzan amesema Kamati ya Uongozi imekutana katika kikao cha pamoja na serikali pamoja na baadhi ya wabunge akiwemo James Mbatia na kukubaliana kwamba Tume ya Uchaguzi ikutane na Wadau wa zoezi hilo wiki ijayo wakiwemo Kituo cha Demokrasia Tanzania TCD kwa ajili ya kupata suluhu ya mchakato huo.

Amesema pia kuwa katika kikao hicho, kamati ya uongozi imeridhika na maelezo ya serikali kuhusu suala hilo na kuiagiza kamati ya Bunge ya Katiba Sheria na Utawala kulifuatilia suala hilo na kupeleka taarifa bungeni siku ya Ijumaa (Februari 6, 2015).

Hata hivyo taarifa hiyo ya mwenyekiti wa Bunge Musa Azzan haijasema ni kiasi gani na lini fedha zitatolewa.