Ijumaa , 5th Sep , 2014

Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho kikwete amesema serikali ina mpango wa kuandaa sera mpya ya elimu ambayo lengo lake ni kuboresha mfumo wa elimu nchini ambayo itakamilika ifikapo 2025.

Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Kauli hiyo ameitoa jana mkoani Dodoma alipokuwa akiwahutubia wazee wa Dodoma ambapo amesema sera hiyo itaambatanisha na suala la kufuta ada kuanzia elimu ya msingi mpaka sekondari na ikiwemo mikakati ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya elimu nchini ikiwemo suala la utoro wa wanafunzi na mimba jambo ambalo linarudisha nyumba utekelezaji wa mpango wa serikali wa matokeo makubwa (BRN)

Aidha Rais Kikwete amesema upo umuhimu wa wazazi kutilia mkazo elimu ikiwemo kuchangia chakula ikiwa ni jitihada za kufanya watoto kupenda shule na kutokomeza tatizo la utoro haswa katika mkoa wa Dodoma.

Wakati huo huo, watu watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi toka nchini Burundi wakiwa na silaha za kivita wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi wilayani kasulu mkoani Kigoma baada ya jaribio la kuteka magari barabara ya Kasulu-Kabondo kushindikana.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Jafari Mohamed amesema tukio hilo limetokea katika pori la mto Malagarasi baada ya watu hao kuingia mtego wa polisi ambao walikuwa wameweka baada ya kupata taarifa kuhusiana na tukio hilo.

Kamanda Mohammed amesema bada ya majambazi hayo kugundua mtego huo walianza kurushiana risasi hali iliyopelekea vifo vya watu hao huku polisi wakifanikiwa kukamata silaha mbalimbali walizokua wakitumia ambazo ni pamoja na bunduki mbili aina ya SMG na AK 47 NA RISASI 64.