Jumanne , 15th Nov , 2022

Imeelezwa kuwa miradi mitatu ya maji iliyojengwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) eneo la Kisesa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, imekumbwa na upungufu wa maji hali inayodaiwa kushindwa kutoa huduma hiyo muhimu kwa wananchi

Wakizungumza mbele ya Mbunge wa Kisesa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Luhaga Joelson Mpina, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Isengwa wilayani humo, wamesema upungufu huo wa maji umeanza kuathiri wananchi hivyo wameiomba Serikali ichukuwe hatua za haraka kuondoa changamoto hiyo.

“Kama hawa vijana wanaotusaidia kwa upande wa maji wanatutosha Meatu na kama hawatutoshi ni vizuri wakaondoka. Kwa sababu gain huwezi kutengeneza (kujenga) mradi mkubwa siku mbimbi, tatu, mwezi mmoja maji hayapo. Ni aibu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wanacheza tu. Mtapambana kutafuta fedha nyingi, watu hawasimamii vizuri, majibu yao ya kijeuri na sisi tunawatizama tu,” amesema Jeremiah.

“Mhe Mbunge (Luhaga Mpina) hebu lichukuwe hili umsaidie mama yetu Samia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mnatakiwa mmsaidie huyu mama ana shida (shauri) sana ya kumtua  mama ndoo kichwani, lakini wasimamizi wake sasa hawaendani naye. Mheshimiwa hii miradi ipo ndani ya jimbo lako, chukuwa kabisa hili ukalisemee,” amesema Shimba.

Kwa upande, wake Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Joelson Mpina, amesema miradi mikubwa mitatu ya maji iliyojengwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imekwama kutoa maji, hivyo amemuomba Waziri anayeshughulikia Maji, Jumaa Awesso, kupeleka haraka timu ya uchunguzi maeneo husika ili kubaini sababu ya changamoto hiyo.

“Maji hayatoki, jambo baya sana. Ule (mradi) wa Lubiga na wenyewe hautoi maji na wa Mwanduitinje hautoi maji, mradi huu wa kwetu wa Isengwa hautoi maji….miradi mitatu. Kwamba pale Mwanduitinje pale (Sh) Milioni 500 (gharama ya ujenzi wa mradi), mradi hautoi maji, Lubiga (Sh) Milioni 800 hautoi maji. Waziri (Wa Maji-Jumaa Awesso) anaweza kutuma wataalamu kuja kukagua kwa kina kuja kujua ni wapi (changamoto ilipo). Labda mashine zilizowekwa ni ndogo, au haziwezi kupampu maji zinavyotakiwa, au chanzo cha maji kule chini hakitoshi. Yaani lazima tupate suluhu na wananchi wapate maji,” amesema Mbunge Mpina.

Hata hivyo, mara kadhaa Uongozi wa RUWASA umeombwa kuzungumzia madai ya miradi hiyo mitatu kushindwa kutoa maji, lakini umeshindwa kufanya hivyo.