Alhamisi , 7th Mei , 2015

Kiongozi Mmuu wa chama cha ACT- Wazalendo Bw. Zitto Kabwe ameishauri serikali kuacha kujadili mchakato wa upigaji wa kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa kwa sasa hadi baada ya uchaguzi mkuu kutokana na mchakato huo kusuasua.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo Bw. Zitto Kabwe.

Akizungumza na East Africa Radio Zitto amesema kuwa mchakato huo hauna faida kwa taifa kwa sasa na ni vyema serikali ikaongeza nguvu kwenye mchakato wa kufanya uchaguzi mkuu na uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

Katika hatua nyingine Zitto amesema serikali isijaribu kuahirisha uchaguzi mkuu kwa kuwa itahatarisha amani ya nchi na pia itakuwa ni kinyume cha Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amewataka vijana kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ubunge na udiwani ikiwa ni pamoja na kujiandikisha kwa wingi ili kuweza kuleta changamoto ya mabadiliko ya kisiasa nchini.

Amesema vijana wanatakiwa kupewa fursa katika nafasi mbalimbali za uongozi ili kuleta mabadiliko katika jamii ya watanzania.

Aidha Zitto amesema katika uchaguzi mkuu mwaka huu pamoja na chama chao kuwa kichanga wamepanga kusimamisha mgombea uraisi, wabunge na madiwani na wengi wao wakiwa vijana katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuleta mabadiliko.