Jumamosi , 28th Mei , 2022

Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekabidhi kwa taasisi nne viwanda 10 ambavyo wawekezaji wake walishindwa kuviendeleza kulingana na mikataba ya mauzo na hivyo malengo ya serikali ya kubinafsisha viwanda hivyo kutotimia.

Taasisi zilizokabidhiwa viwanda hivyo ni Mamlaka ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB).  

Agosti, mwaka jana Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, wakati huo, alitangaza na kutoa maelekezo kuhusiana na Viwanda 20 vilivyorejeshwa serikalini na kusema viwanda 10 vihamishiwe katika Taasisi za umma na Viwanda 10 vitafutiwe wawekezaji wengine kwa njia ya zabuni.

Akikabidhi viwanda hivyo jana jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto aliwapa wakuu wa taasisi hizo wiki tatu kuhakikisha kwamba wanawasilisha mpango kazi ambao utafuatiliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Viwanda 10 ambavyo vimeelekezwa kuhamishiwa katika taasisi hizo ni TPL Shinyanga Meat Plant ambacho ni cha nyama, Mafuta Ilulu (Lindi), kiwanda cha kubangua korosho cha Nachingwea Cashewnut (Lindi), Mkata Sawmill Limited na Sikh Sawmill Limited (Tanga), National Steel Corporation cha Dar es Salaam na  Mbeya Ceramic Ltd. Vingine ni Mang’ula Mechanical & Machine Tools (Morogoro), Mwanza Tanneries (Mwanza) na TPL Mbeya.