Jumamosi , 27th Aug , 2022

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuangalia namna bora ya kuliboreaha eneo la Laitoli lenye nyayo zinazosadikiwa kuwa ni za binadamu wa kale walioishi miaka milioni 3.6 iliyopita ili kuiingizia Serikali mapato

Aidha, Balozi Dkt. Chana ameongeza kuwa kazi aliyoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya Utalii kupitia Filamu ya The Royal Tour inapaswa kuungwa mkono kwa Idara na Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha, kuendeleza na kubuni vyanzo vipya vya mazao ya utalii ili kukidhi mahitaji na wingi wa watalii wanaoingia nchini.

Kwa upande wake Naibu Kamishna (Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii) Dkt Christopher Timbuka, amesema Mamlaka hiyo itayafanyia kazi maelekezo ya Waziri Balozi Dkt Chana ili eneo hilo liweze kukidhi kiu kubwa ya Watalii wanaotembelea Hifadhi hiyo.

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amefanya ziara ya kikazi katika eneo hilo ili kupata taarifa za maendeleo ya uhifadhi na uendelezaji wa eneo hilo muhimu kwa historia ya binadamu na Urithi wa Dunia.