Jumanne , 10th Mei , 2022

Shahidi wa kwanza katika kesi inayomkabili Mfalme Zumaridi na wenzake ameieleza Mahakama kwamba alipofika kanisani kwa ajili ya kumchukua mtoto aliyekuwa akiishi hapo wafuasi wa Zumaridi walianza kumpiga Askari polisi aliyekuwa naye huku wakiunguruma.

Mfalme Zumaridi akiwa Mahakamani

Akiongozwa na Wakili wa serikali Emmanuel Luvinga, shahidi huyo ambae ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Christina Mwisongo, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza kuwa Februari 22, 2022, alipokea amri ya Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni ya kumtaka aende nyumbani kwa mchungaji Zumaridi kuchukua mtoto ambaye jina lake limehifadhiwa aliyekuwa akiishi nyumbani kwa Zumaridi.

Mbele ya Mahakama hiyo shahidi huyo amesema  kuwa baada ya kufika nyumbani kwa Zumaridi akiwa ameongoza na Askari polisi hawakufunguliwa geti la nyumba hiyo hatua iliyowafanya kupitia mlango wa nyuma na kuingia ndani ambapo hawakupewa ushirikiano wa kutosha baada ya kukuta watu wengi wakisali na kuunguruma.

Wakili wa upande wa utetezi Erick Mutta, alimuuliza shahidi huyo kwanini alienda kanisani kwa Zumaridi badala ya nyumbani kwake, shahidi huyo akajibu kwamba walimuuliza baba wa mtoto huyo na kuwaambia kwamba mwanaye kwa wakati huo alikuwa kwa Zumaridi.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi  Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Monica Ndiyokobora, ambapo imepangwa kusikilizwa tena tarehe Mei 19 ambapo mashahidi wengine wataendelea kutoa ushahidi wao.

Inadaiwa kuwa February 23, mwaka huu  katika eneo la Buguku, Buhongwa wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, washtakiwa hao kwa pamoja walimshambulia Askari James Mgaya katika sehemu mbalimbali za mwili na kumzuia kutekeleza majukumu yake.