Alhamisi , 10th Sep , 2015

Mgombea urasi wa Zanzibar kupitia chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema atahakikisha anaimarisha uchumi wa visiwa hivyo akipata ridhaa ya kuwa Rais akishinda uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Katibu Mkuu wa CUF ambae pia mgombea Urais wa UKAWA kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,

Akiongea visiwani humo katika viwanja vya kibanda maiti wakati wa uzinduzi wa kampeni za CUF, Sharif Hamad amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma za msingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa wananchi hususani kwa vijana.

Sharif Hamadi amesema ataimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kufungua benki ya uwekezaji kwa watanzania ili kuondokana na wimbi wa umasikini.

Kwa Upande wake Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Mh. Edward Lowassa amewataka wazanzibar kuchagua UKAWA ili kuweza kubadilisha hali za kiuchumi za watanzania.

Mh. Lowassa amesema Maalim Seif ameanza safari ndefu ya mabadiliko katika visiwa hivyo kwa hiyo Wazanzibar wamchague ili kumalizia kazi aliyoanza katika serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.