Ijumaa , 16th Jun , 2017

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ametoa onyo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaoitumia vibaya mamlaka yao ya kuwakamata na kuwaweka ndani watu kwa saa 48.

Simbachawene ametoa kauli hiyo leo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maaalum, Cecilia Pareso kuhusu Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaoamuru kukamatwa na kuwekwa ndani kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa vijiji bila sababu za msingi.

"Ni kweli sheria hii ya mikoa inatoa mamlaka kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuweza kumkamata mtu katika mazingira ambayo wanaamini kwamba mtu huyo ama anatenda kosa la jinai ama anafanya kitendo chochote kinachovunja amani na utulivu. Asikamatwe mtu kwa ajii ya 'show', asikamatwe tu kwa kuonesha wewe una madaraka lazima akamatwe mtu huyo kama kweli kitendo chake kinahatarisha amani na utulivu" alisema Simbachawene.

Pamoja na hayo, Simbachawene amesisitiza kwa kusema "Wakuu wetu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya kwa kutumia sheria hii wawe makini kuhakisha kwamba wanaitumia kama vile sheria inavyotaka".