Jumatano , 1st Oct , 2014

Wakili na mwanaharakati maarufu nchini Tanzania,Harold Sungusia, ametoa maoni yake kuhusu zoezi linaloendeelea katika bunge maalumu la upigiaji kura kwa katiba inayopendekezwa.

Mwanaharakati na wakili maarufu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu - LHRC Harold Sungusia (kulia).

Katika maoni yake, Sungusia ameelezea kusikitishwa na namna baadhi ya wanaharakati waliogeuka vigeugeu na usaliti kwa kushiriki zoezi hilo na kushindwa kutetea maslahi ya Watanzania.

Akizungumza katika mahojiano na EATV, Sungusia amesema kinaochoendelea katika bunge hilo hivi sasa ni kutafuta uhalali wa theluthi mbili zinazotakiwa kupitisha katiba hiyo, kitendo alichokifananisha kuwa ni sawa na timu inayoamua kupanua goli la adui yake kwa lengo la kutaka ifunge kirahisi.

Katika hatua nyingine, mtandao wa Jinsia nchini Tanzania (TGNP), umetoa maoni kuhusu rasimu ya tatu ya katiba inayopendekezwa kuwa imeweza kuanisha masuala ya jinsia kwa asilimia 90 ikiwa pamoja na kupitisha vipengele 12 vilivyoainishwa ikiwemo kubanwa kwa vyama vya siasa.

Akizungumza jijini Dar es salaama katika Kongamano la wazi lililohusu rasimu inayopendekezwa na bunge maalumu la Katiba Prof. Ruth Meena, amesema asilimia kubwa ya nguvu kazi hasa vijijini ni wanawake na kueleza kuwa haki za usawa wa kijinisia ya 50/50 itasaidia wanawake kupata haki zao za msingi ikiwemo haki ya kumiliki ardhi.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa TNGP Bi Lilian Liundi amesema zipo changamoto zilizojitokeza ikiwemo baadhi ya vipengele kutowasilishwa katika rasimu hiyo ikiwemo suala la ukomo wa uongozi wa wabunge na suala la mgombea binafsi.

Kwa mujibu wa Liundi kuwepo kwa nafasi ya mgombea binafsi kutawasaidia wanawake ambao wengi wao hawana uanachama katika vyama vya siasa kupata fursa ya kugombea nafasi za uongozi ikiwemo ya Urais.