Jumatatu , 25th Aug , 2025

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linafanya uchunguzi kuhusiana na tukio la mtu mmoja aitwaye Bakari Halifa Daud (18) mkazi wa Sombetini Jijini Arusha kujeruhiwa kwa kupigwa risasi mguuni.

Akitoa taarifa hiyo leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 23, 2025 muda wa saa 5:30 usiku huko katika maeneo ya Sombetini Jijini Arusha.

Kamanda Masejo ameendelea kufafanua kuwa wakati Abdulaziz Abubakari (30) mkazi wa Levolosi Jijini Arusha akiwa anashuka kwenye gari alidai kutaka kuvamiwa na Bakari Halifa akiwa na mwenzake kwa kutumia silaha ya jadi hali iliyopelekea kutumia silaha aliyokuwa nayo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu wawili kuhusiana na tukio hilo ambapo limesema bado linaendelea na uchunguzi.