Jumanne , 18th Jan , 2022

Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto mkoa wa Ilala Elisa Mugisha, amesema kwamba taarifa za kuungua kwa soko la Karume walichelewa kuzipata kwani wangezipata mapema wangeweza kuokoa athari iliyojitokeza.

Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto mkoa wa Ilala Elisa Mugisha

Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 18, 2022, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, na kusema licha ya kufika na kukuta moto umekua mkubwa lakini pia mazingira ya sokoni hapo si rafiki kwani hakukuwa hata na nafasi ya kupitisha gari.

"Watu waliuona moto mapema, lakini wakaanza kupambana na moto na sisi tumepata taarifa saa 9:12 usiku, tumefika pale saa 9:30, sisi tuko mbali kidogo tunauona moto umeshakuwa ni mkubwa, pale tarifa hazikutolewa mapema," amesema Kamanda Mugisha.

Aidha ameongeza kuwa, "Kulikuwa na magari manne ya kuzima na tulizunguka sana kulingana na mazingira ya pale, taarifa ingetolewa mapema tungeudhibiti, na waliokuwepo walipoona moto umewashinda wakaanza kuokoa mali zao,".