TAKUKURU yakamata vigogo 7 uhujumu uchumi

Jumamosi , 17th Nov , 2018

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Tabora imewapandisha kizimbani Watumishi 7 wa halmashauri 3 za mkoa wa Tabora kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.

Makao Makuu TAKUKURU.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa taaasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Tabora, Mogasa Mogasa amesema kuwa katika kipindi cha Julai-Septemba 30 mwaka huu, jumla ya malalamiko 28  ya rushwa yalipokelewa na Taasisi hiyo na kufunguliwa mashtaka na sita kati yake yamefikishwa mahakamani.

Mogasa amewataja watuhumiwa wa shauri hilo la uhujumu uchumi kuwa ni Bikilile Mahyenga (Kaimu Mweka hazina)  na Andrew Ndaba (Mhasibu) wanaokabiliwa na mashitaka mawili ya kughushi na kupokea rushwa.

Amesema kesi nyingine ni cc na.74/2018 dhidi ya Stephen Nyanda aliyekuwa Mhandisi wa halmashauri ya wilaya ya Uyui ambaye shauri lake lipo kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Tabora Sarafina Nsana na linatarajiwa kutajwa Novemba 28 mwaka huu.

Mogasa amemtaja mtuhumiwa mwingine aliyefikishwa mahakamani kuwa ni Emanuel Mwakasumule aliyekuwa Katibu wa Baraza la Ardhi kata ya Ziba wilaya ya Igunga ambaye anakabiliwa na kesi ya rushwa na. 1/2018.