Ijumaa , 7th Oct , 2022

Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Anne  Makinda amesema serikali kupitia tume za taifa za Takwimu Tanzania bara na visiwani Zanzibar imelenga  kutumia takwimu za sensa kutoa elimu kwa umma  juu ya umuhimu wa kujiajiri ili kuondokana na tatizo la ajira hapa nchini

Makinda  amesema hayo wakati alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa zoezi la Sensa ya watu na makazi ambalo  lilifanyika Agosti 23 mwaka huu ambapo  amebainisha kufanikiwa kwa zoezi hilo zaidi  ya asilimia 90 kote nchini. 

Awali akieleza namna sensa ilivyofanyika kwa mkoa wa Tanga mratibu  wa mkoa huo Tony Mwanjota amesema kuwa wameweza kufanikiwa kuhesabu kaya kwa asilimia 95 na kuyafikia majengo yote, kuwezesha kutoa elimu na hamasa kwa wananchi  ambayo imepelekea ushirikiano mkubwa uliochangiwa na viongozi wa  serikali dini na siasa

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Tanga Omari Mgumba  ameeleza kuwa  wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan  ya kutenga maeneo maalumu  kwaajili ya kilimo ili kutumia sekta ya Kilimo katika kuwakwamua wananchi na umasikini na kuwa na chakula toshelevu wakati wote ili kuweza kuchangia pato la taifa.

Katika sensa ya watu  ya mwaka 2022 mkoa wa Tanga ulikadiria kuhesabiw jumla ya Kaya 649,591  lakini ni kaya 617,431 pekee zilizohesabiwa  na kufanya kufikia asilimia 95 huku  sensa ya majengo ikifanikiwa kwa asilimia mia moja na hatimaye kuhesabu nyumba  zipatazo 730,934.