Jumanne , 18th Dec , 2018

Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussein Ruhava amekiri kuwepo kwa sintofahamu juu yauwepo wa mtu anayefahamika kwa jina la 'Teleza' ambaye amedaiwa kuwaingilia kimwili wanawake wasiokuwa na waume usiku kwenye wilaya hiyo bila ridhaa yao.

Wananchi wakiwa kwenye taharuki

Kwa mujibu wa Meya huyo, malalamiko juu ya uwepo wa 'Teleza' yalifika kwenye Baraza la Madiwani ambapo waliagiza Jeshi la Polisi kulishughulikia suala hilo.

Akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Breakfast cha East Africa Redio Meya Ruhava amesema tukio hilo halina uhusiano wowote na imani za kishirikina bali vilikuwa ni vitendo vya kiuhalifu.

"Ni kweli mwanzoni mwa mwaka huu tulipokea taarifa ya kuingiliwa kwa wanawake bila ridhaa yao, lilitufikia kwenye vikao vya Baraza la Madiwani na tuliamuagiza OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) ayafanyie kazi na walijitahidi kulizima hilo zoezi." amesema Meya Ruhava

"Walipochunguza zaidi wakawagundua watu wanaofanya vitendo hivyo na waligundua kuwa halina uhusiano wowote na vitendo vya kishirikina, bali kuna vijana ndiyo walikuwa wakilifanya na juzi alhamisi na ijumaa lilibuka tena na Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta vijana hao," ameongeza Meya huyo.

Wiki iliyopita kupitia Mkuu wa wilaya ya Kigoma Mjini Samson Anga alieleza kutolitambua suala hilo.