Alhamisi , 15th Nov , 2018

Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), kinakwenda sambamba na kasi ya Rais John Magufuli katika kuziba mianya ya uwepo wa rushwa katika utumishi wa umma ili kurahisisha suala la uwekezaji nchini.

Makao makuu ya TIC.

Hilo limebainishwa na Afisa uwekezaji mwandamizi anayehusika na sera, utafiti na mipango kutoka TIC, Brendan Maro, kupitia MJADALA wa East Africa Television leo Novemba 15, 2018, ambapo amesema kwasasa suala la uwekezaji ndani ya TIC ni rahisi sana kwasababu haichukui muda na wala hakuna usumbufu.

''Mazingira ya ufanyaji biashara yameboreshwa kwa kiasi kikubwa sana ikiwemo kuwepo kwa miundombinu wezeshi kwa wawekezaji lakini pia uwepo wa wepesi wa kukamilisha zoezi lenyewe ndani ya TIC ambapo kwasasa nidhamu ya utumishi wa umma ni kubwa hata mianya ya rushwa haipo'', amesema.

Aidha Bw. Maro ameweka wazi kuwa tayari kituo hicho kimeshabaini uwepo wa elimu hafifu juu ya suala la uwekezaji ambapo wengi wanafikiri mwekezaji ni kutoka nje kumbe uwekezaji ni fursa kwa wote na upo mpango wa kuanza kupeleka taarifa sahihi kwa wananchi.

Pia ameongeza kuwa katika kuhakikisha wanawafikia wananchi wote kituo hicho cha uwekezaji kimeongeza ofisi za kikanda ukiacha Dar es salaam kwasasa kuna ofisi Dodoma na Kigoma.