Jumatatu , 22nd Feb , 2016

Serikali imesema kuwa imekusanya zaidi ya shilingi trilion moja za kodi katika mwezi Februari pekee.

Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Servacius Likwelile ambaye amesema kuwa hali hiyo imetokana na kuboreshwa kwa utaratibu wa ukusanyaji wa mapato nchini na kupelekea makusanyo hayo kuvuka lengo lililowekwa.  

Likwelile amesema hayo hii leo wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam  na kuongeza kuwa fedha hizo zimegawiwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia walimu walioko vyuoni, kumalizia ujenzi wa jengo la Mloganzila, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, miradi ya maji, Shirika la Reli na Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini.

Kwa upande wake katibu mkuu wizara ya elimu Bi Maimuna Tarishi Kibenga amesema kuwa fedha waliyopewa wataitumia kuboresha mafunzo ya walimu walioko vyuoni hasa katika kujifunza kwa vitendo zaidi ili waweze kuwa na mbinu mpya za kuwafundisha wanafunzi na kukuza sekta ya elimu nchini.

Aidha katibu mkuu wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto amesema kuwa wataboresha jengo la Mloganzila ili kutoa nafasi kwa wanafunzi madaktari na wauguzi waweze kuwa na sehemu nzuri zaidi ya kujifunza kwa vitendo.